Inatafuta...

SIMULIZI : Kitanzi Au Bastola - 03 Sehemu Ya Tatu

Kitanzi, Kisu au Bastola - 03


ILIPOISHIA
Jasho jingi lilimtiririka na kufuatiwa na maumivu makali ndani ya kifua chake. Mapigo ya moyo yalimuenda kwa kasi na kusimama kwa mara moja. Ghafla nguvu zake zilimuishia akadondoka na kuzirai akiwa peke yake chumbani. Je, nini kitatokea? ENDELEA…
Salima alitembea haraka akielekea dukani kwa Dedan. Moyoni akiwa na malengo makuu mawili, kuichukua simu yake aliyoiacha kwenye chaji usiku wa jana yake na kumfungukia Dedan kuhusu dukuduku aliloliweka rohoni kwa muda mrefu.
Njiani kote moyo wake ulimdunda kwa kasi akihofia ni nini Dedan atamjibu kama atamwambia hisia zake. Kile kiroho cha nighairi leo nimwambie kesho kilizidi kuisumbua nafsi yake.
Akaona kama kila siku ataendelea kuogopa na kuishia kusema atamwambia kesho, basi kwa hakika hatamwambia daima na zaidi ataendelea kuumia tu na kesho zisizofika.
“Leo lazima kieleweke,” Salima alijipa moyo huku akijiangalia vizuri kuanzia juu mpaka chini jinsi alivyopendeza. Akahakikisha anatembea mbali na barabara akihofia vumbi la magari lisije likamchafua.
Hakuwahi kujisikia hali hii kwa mwanaume yeyote kabla hajakutana na Dedan, lakini siku hiyo alishindwa kabisa kujizuia kujipodoa na hata kupitiliza. Asubuhi alipokuwa bafuni alitumia takriban nusu saa kuhakikisha alikuwa msafi kila kona ya mwili wake.
Hata alipokuwa chumbani mwake, alijishangaa akitumia muda mwingi kucheza mchezo wa vua vaa kwa kila aina ya nguo mpaka alipoipata suruali yake adimu aliyoiandaa rasmi kwa tukio muhimu kama hilo.
Kwa kuwa alikuwa mgeni wa mavazi ya kubana, alijishangaa baada ya kuona ukubwa wa hipsi zake na jinsi zilivyojichora vema nje ya suruali. Alitembea huku akijiangalia kila hatua aliyoipiga.
Juu alivaa kiblauzi cha pinki kilichoendana vizuri na rangi ya ngozi yake ya kahawia. Kifua chake kilikuwa wazi sehemu kubwa na kukifanya kivutie maradufu huku kichwani akiwa amevaa wigi la rangi nyeusi akizifunika nywele zake zisizoijua saluni kwa muda mrefu.
Ilikuwa wazi kwamba uzuri wake siku zote ulijificha kutokana na jinsi alivyokuwa akijiweka, lakini siku hiyo hata yeye mwenyewe alijishangaa na kujikubali kwamba wakiitwa warembo kumi hakika na yeye ataitika.
Njiani kila mtu alikuwa akimuangalia kwa mtazamo mpya. Yeye pia alionekana akiupenda sana muonekano huo. Akazidisha mikogo na kujifanya kama ameizoea hali hiyo japo moyoni alijaa aibu tele kwa ugeni wa kila alichokivaa siku hiyo.
Akiwa njiani alifungua kipochi chake na kutoa kioo kidogo akihakikisha poda na rangi aliyoipaka mdomoni imesambaa vizuri. Akajilazimisha kutabasamu ili kuondoa mikunjo yoyote ya huzuni kwenye uso wake japokuwa haikuwepo.
Akiwa anakaribia kona ya mwisho kutokea kwenye kibanda cha Dedan, Salima alibana kwenye kona na kuhema kwa nguvu. Akajipulizia marashi kwa mara ya mwisho. Akajitokeza na kuanza kutembea taratibu huku akiangalia ni wapi alipo Dedan ili amroge kwa muonekano wake alioenda nao siku hiyo.
Kwa mbali, alishangaa kuona kibanda kimezungukwa na watu wengi ambao bila shaka walikuwa wateja wa Dedan, kwani wengi huwa na mazoea ya kuacha simu na betri zao usiku mzima kwenye chaji kwa ahadi ya kwenda kuzichukua siku itakayofuata.
Salima alishangaa kuona mpaka saa nne, bado ofisi ya Dedan ilikuwa haijafunguliwa. Alihisi kuna walakini kwani kwa jinsi alivyomjua Dedan, hakuwahi kumwona hata siku moja akikosa kufungua ofisi yake mapema pasi na sababu maalumu.
“Pengine anaumwa!”alistaajabu Salima huku akiukaribia umati uliojaa nje ya duka la kijana huyo ili angalau ajue nini kilichokuwa kikiendelea.
“Huyu jamaa vipi leo? Kuna mtu anayepajua nyumbani kwake? Sisi tunachelewa kazi zetu bwana!” Hayo ndiyo maneno aliyosikia yakisemwa na watu walioshindwa kuvumilia huku wengine wakidiriki kuyapuuza mema yote waliyofanyiwa na Dedan kwa kumtuhumu huenda akawa amewatia changa la macho na kutoroka na fedha na simu zao.
Presha ikaanza kumpanda Salima. Akapitiliza bila hata kupiga hodi na kuingia moja kwa moja hadi ndani ya nyumba kubwa yenye vyumba vingi vilivyotenganishwa na varanda nyembamba.
Akahesabu vyumba kuanzia mkono wa kulia na kugonga mlango wa chumba cha tatu. Akagonga tena na tena bila mafanikio.
Hofu ikaanza kumpanda kadiri alivyokosa majibu ya hodi zake. Akachungulia kwenye kitasa akaona ufunguo ukiwa ndani ya kitundu cha mlango.
Je, Dedan amepatwa na nini?
Akahisi huenda Dedan alijifungia kwa makusudi kabisa na pengine alikuwa amelala na mwanamke mwingine ndiyo maana alishindwa kumfungulia mlango. Hasira na wivu vilimjaa Salima, akaanza kujilaumu kwa kila kitu alichojisumbua kwa ajili ya Dedan kwa siku hiyo. Nguvu za miguu zilimuishia, akajikuta akikaa chini na kuuegemea mlango wa chumba cha Dedan akilia. Machozi yalimtoka mpaka yakamkauka kwa mapenzi yaliyozidi kipimo. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake, akawa hajitambui kabisa. Akawa kama mtu aliyechizika, huku mapenzi yakiwa ndiyo sababu kubwa ya uchizi wake.
Akaona hapana, ni lazima ahakikishe ukweli wa kile alichokuwa akikiwaza. Akajibanza pembeni kwenye kona akitega sikio juu ya ubao wa mlango akikusudia kusikiliza kila tendo lililokuwa likifanyika mle chumbani.
Japokuwa kulikuwa kumetawala ukimya wa hali ya juu, lakini kwa upande wake alisikia sauti kubwa zikitoka chumbani tena kwa ufasaha kabisa. Aliisikia sauti ya huyo mwanamke aliyeamua kumpachika jina la malaya na ile ya Dedan zikisemezana kwa maneno ya faragha kana kwamba walikuwa kwenye mapenzi mazito sana. Kwa sikio lake alimsikia vyema huyo malaya akizungumza kwa lugha laini na kwa sauti ya kubana pua.
Wakati huo akili ya Salima ilikuwa ikimpeleka kama aliyokuwa akitaka mwenyewe, ilimtoa kutoka kwenye ulimwengu wa uhalisia na kumtupa sehemu mbali kabisa kwenye ulimwengu wa dhahania ambao laiti kama ungepewa jina ungeitwa Ulimwengu wa Watu Wenye Wivu wa Kipumbavu. Ulimwengu ambao wenye wivu usio na maana wote wangekutana huko na pengine kuanzisha serikali huku Salima akiwa rais wao. Akawa akiwaza kitu na mara moja kinakuwa kweli, sawa sawa na kuwaza bahari na ghafla mbele yako inatokea.
Macho ya Salima yakaanza kujaa ukungu huku machozi yakimlengalenga kwa hasira na wivu, ingawa hakuwa mpenzi wa Dedan rasmi, lakini aliumia sana. Alijihisi kama vile alikuwa akiibiwa mali yake. Siku zote alitamani kuwa mwenye haki juu ya mwili na akili ya Dedan na siyo mwanamke mwingine yeyote. Aliamini amezaliwa si kwa ajili ya mwanaume mwingine zaidi ya Dedan Magesa. Moyo wake ulikuwa huko na daima aliapa kulipigania penzi lake.
Alijikuta akiwaza mambo mengi ambayo kiukweli yote yalikuwa ya kuhisi tu na laiti kama angejua yaliyomkuta Dedan huko chumbani hakika nafsi yake ingemsuta kwa kumuhukumu kwa uongo bila kujua ukweli; na hata kama ingekuwa kweli kwamba Dedan alikuwa na mwanamke chumbani kwake, yeye Salima alikuwa ni nani mpaka aingilie maisha yake? Hakuwa mpenzi wake, wala rafiki yake. Alikuwa mteja wake tu hapo dukani, sasa kwa nini ajifanye anajali sana?
Alifikia kipindi akawa hawezi kabisa kuuzuia uchizi wake, akasimama na kurudi nyuma hatua kadhaa na kuurukia kwa nguvu mlango ambao tayari ulikuwa umeshaanza kuliwa na mchwa. Mlango ukajiachia kwa kukatika katikati huku vipande viwili vikining’inia kwenye bawabu,“ lolote na liwe,” aliwaza Salima.
Ilimchukua dakika kadhaa kuzinduka katika bumbuwazi alilokuwa nalo. Hakukuwa na huyo mwanamke malaya aliyekuwa akimuwaza wala hakukuwa na Dedan hapo kitandani, ila kuna kitu mfano wa mtu upande wa pili chini ya kitanda.
“Ni nini…Ah! Ni nani… Dedan! Dedan! Nini tena? We Dedan!” Salima alijikuta akipiga makelele yaliyochanganyika na kilio baada ya kumuona Dedan akiwa hajitambui huku akitokwa na mapovu mdomoni.
***
“Mimi ni Salima unanikumbuka?”
“Mmm...”
“Mimi ni mpenzi wako Salima, haunikumbuki?”
“Mmm…”
“Jana tu nilikukumbusha jina langu, kwa nini unanisahau jamani!”
“Mmm…”
Kila alichokiongea alijibiwa: “Mmm…” Mpaka akachoka, akaamua kukaa kimya akimwangalia tu.
Hakuna rafiki wala ndugu yake hata mmoja aliyejua kama anaishi na mwanaume. Aliifanya siri kubwa moyo wake ukawa sanduku pekee la kuihifadhi.
Pamoja na furaha yake mpenzi wake hakuwa na uwezo wa kufanya kitu chochote. Siku nzima alishinda amekaa au amelala kitandani kama zezeta..
Like Page Yetu Kuendelea Kupata simulizi Hapa chini
https://www.facebook.com/uwanja007

Changia Maoni Yako Hapa

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright Bongo Choice | Modified By Bongo Choices
Back To Top