
Taarifa
nilizo nazo ni kwamba waishiwa ni mabingwa wa kutoroka mjengoni hasa
wakati wa mijadala inayohitaji kutumia bongo. Nani anapenda kuumiza
bongo lake wakati anaweza kuchepuka mijadala ya kuboa ikaisha akacha
akazoa uchache na kwenda kujinoma? Je namna hii mnamkomoa nani zaidi ya
kaya wajameni? Hata hivyo, tangu kaya igeuzwe No Man’s Land aka Shamba
la Bibi nani anajali?
Hata
hivyo, kwa kuelewa umuhimu wa chata la Mzee Jose Walioboa walilonyonga
wakota kwa kutaka kuzuia ufisadi wao, msishangae kusikia wahishimiwa
waishiwa wakifanya utoro. Wamekuwa wakifanya
hivyo hata wengine kuuchapa mjengoni huku wakianikwa na vyombo vya umbea
udenda ukiwatoka na wengine kukoroma na kushua kwa kisambaa yaani kutoa
hewa mbaya. Bila kuua ili chata mbona wengi
wangekoma na kukomaa. Kama wanakaya walitaka kuwatimua hata kabla ya
msimu wao wa uishiwa haujaisha wanapoboronga viherehere wakawakingia
kifua unategemea nini? Hivyo, haka kamchezo ka kukacha mjengo au kukaa
mle kama masanamu bila kuchangia kataendelea. It is a lucrative business of siphoning boozers’ dosh.
Acha niseme kimombo kidogo kuonyesha kuwa sikughushi wala kupewa ya
dezo kama jamaa zangu madaktari na maporofwesa wa urongo na ukweli. Jei
nonihino upo mpenda sifa?
Kwa
vile waishiwa wanapotoroka mjengoni wanaishia kwenye mabaa na majumba
ya kulala wageni kufanya vitu vyao, lazima niwapongeze kwa kupata
kanywaji na starehe au vipi? Naona yule anasoma na kutikisa kichwa. Yule
muishiwa naona anaanza kuchukua notebook ili aende kuchongea gazeti
hili kwa kuwapa vipande vyao. Usijihangaishe. Ninaposema wanakwenda
kwenye nyumba za wageni simaanishi wanakwenda kufanya majamboz zaidi ya
kuuchapa usingizi. Hivyo, huna haja ya kupandwa na presha bure kuwa
nimetukana au kugusa pasipoguswa. Waende huko wafanya majamboz au
inanihusu nini wakati miwaya ipo inawangoja? Wakitaka waende au waache
shauri yao. Kinachonihangaisha ni huu wizi wa mchana watoto hawa
wanaofanya. Kama wamechoka uishiwa si waache kuliko kutelekeza majimbo
yao? Walichaguliwa kuwakilisha walevi siyo kwenda kufanya ulevi na utoro
ati.
Nawapongeza
waishiwa si kwa kuibia walevi wala kujiweka hatarini kuukosa ulaji
kwenye uchaguzi ujao hasa baada ya kufichuka uhovyo wao kuwa kumbe
hawawakilishi walevi bali kwenda kujifanyia mambo yao huku wakizoa
mshiko! Nawapongeza kwa vile wamenusurika na bonge ya zali kama si sanga
au vipi? Hata hivyo, you are not out of woods yet folks. Hili
nadhani kwa walevi halivumiliki. Lazima kwenye uchaguzi ujao mwezi wa
kumi wapige watu chini tena kwa kishindo cha ki-Tsunami. Najua wengi
wanajipa moyo kuwa watachakachua kama walivyofanya mwaka 2010. Thubutu,
mkijaribu kitaumana kiasi cha kuchimbika bila jembe. Patakuwa hapatoshi
maana walevi wameishachoshwa na mchezo huu wa kichovu mchafu.
Kama
si mama kipaza sauti kuwakingia kifua chake, ningewalima barua waandike
maelezo juu ya kwanza, walipokuwa, walichokuwa wakifanya na kwanini
wasipigwe bakora au mambo yao kuweka hadharani ili umma uwajue walivyo
wa hovyo.
Pili,
ningeamuru mshiko wote waliokwishazoa warejeshe tena kwa kulipa na
interests kwa muda waliokaa nao. Ambao wangeleta gozigozi ningeamuru
mashangingi yao yakamatwe na kupigwa mnada hapo hapo bila kuwapa muda.
Hata hivyo, ni ngedere gani anaweza kumfanyia kweli nyani wakati wote
lao moja yaani kuiba mahindi?
Tatu, ningeandika barua ya onyo na kwa watoro ili iwe kwenye kumbukumbu za mjengo kuwa walitenda jinai hii.
Nne,
ningesambaza waraka kwenye majimbo yao kuwataarifu wenye jimbo kuwa
hawana mwakilishi bali mtoro wa kawaida anayetumia muda na dhamana yao
kufanya mambo yasiyo na maana.
Tano,
ningehakikisha vyombo vya habari vinapewa orodha yao na picha zao ili
vichapishe walevi wawajue na kuwatahadhari kwenye uchaguzi ujao.
Kwa
vile yote haya hayakufanyika, kwanini nisiwapongeze waishiwa kunusurika
kupatikana hata kuutema ulaji kama yule jamaa yangu Mzito Kabwela
aliyejitiatia akaishia kupigwa kadi nyekundu na kuuacha ulaji wakati
akiuhitaji.
Lo!
Nilitaka kusahau kuwapa inshu. Mna habari kuwa waishiwa wanaosemekana
walitoroka mjengoni kwa wingi walikuwa wapi? Kuna shushushu amenitonya
kuwa walikuwa wamekwenda kwenye maadamano ya kumtaka fisadi fulani
agombee ukuu ili awabamize mkenge walevi kama hana akili nzuri. Kwa vile
waliamini kuwa jinai yao ya kutubambika mkenge mwingine inaweza kupita,
walijiamini kwenda wakijua mkuu mpya atawakumbuka wale watakaotoswa na
walevi kutokana na kuwa na nafasi bwerere za kujaza kama vile ukuu wa
wilaya na mikoa, ubalozi, uwaziri ambavyo vimegeuka uchochoro wa
kupachikia washikaji zao. Hata hivyo, lazima niseme wazi. Kama fisadi
huyu atafanikiwa kugombea na baadaye akaupata ukuu basi mwenzenu
nitajinyotoa roho kabla ya kuishi chini ya kidhabu huyu. Uchafu wa
kisiasa, sanaa, ujambazi na uchangudoa wa kila aina vimenitosha. Lazima
nijiondokee mapema kama mzee Mchonga ili nisishuhudie makufuru
yanayoweza kuniua kwa sononi.
Ngoja.
Naona yule muishiwa anaruka ukuta wa mjengo kuelekea Short time Nyumba
ya wageni. Naona na yule mwingine anakata mbuga kuelekea baa ya Mama
Coltide akastue kidogo. Naona yule naye ana msokoto wake wa ganja
anakwenda uchochoroni kupata stimu kama alivyowahi kusema brother
Jobless Nduguy kuwa waishiwa wanavuta mibangi na kubwia miunga nao
wasikanushe.
Hakika
kuna haja ya kuwapongeza wahishimiwa waishiwa kwa kuonyesha sura na nia
zao halisi. Kazi kwa walevi kutafakari kuwa wenzenu wanakwenda kule
kujiwakilisha na si kuwawakilisha. Hivyo, ufikapo mwezi wa kumi lazima
muachane na ulevi na mibangi. Badala yake mchunguze nani anaweza
kuwawakilisha mjengoni bila kutoroka, kuupiga usingizi, kukoroma,
kushua, kutchangia hoja au kutoa upupu anapopata nafasi ya kuchangia.
Chanzo: Nipashe Machi 28, 2015.
Post a Comment