Inatafuta...

SIMULIZI : Kitanzi Au Bastola - 01 Sehemu Ya Kwanza.

Bongo Choice Simulizi Kitanzi Au Bastola

KITANZI AU BASTOLA
SEHEMU YA KWANZA
SIMULIZI YA KUSISIMUA
ANATEMBEA akiwa anapepesuka kwa ulevi uliomjaa kichwani. Amelewa chakaliii, pombe zikimdanganya na kumfanya asiwe na hofu hata kidogo kukatiza kona hatari za mitaa ya Songasonga.
Laiti kama angekuwa na akili zake timamu asingediriki hata kuwaza kupita peke yake usiku huo kwa kuwa anazijua vema sifa za mtaa wake.
Roba za mbao, ubakaji na mara nyingine kesi za mauaji ndiyo mambo makubwa yanayozifanya hata serikali za mitaa na wilaya ziuangalie kwa jicho la tatu pekee mtaa huo. Lakini usiku wa leo, saa nane hiyo, Dedan Magesa anapita bila wasiwasi wowote, mkononi akiwa amekumbatia kopo la pombe ya kienyeji maarufu kama mataputapu.
“Muuuvu bichii geliatu weiii. Muuuvu bichii geliatu weiii,” alijiimbia wimbo wake aliokuwa akiurudiarudia kiitikio tu tena kwa sauti mbaya ya kilevi kinachotia kichefuchefu hata kukisikiliza.
Taratibu Magesa aliyoyoma akipita karibu kabisa na kona na vichochoro kadhaa vyenye sifa mbaya sana za uhalifu. Kama vile mkono wa Mungu ulikuwa juu yake siku hiyo, alifika nyumbani salama salimini. Akafungua na kufunga mlango wa chumba chake kwa umakini mkubwa kisha akajitupa kitandani kwa nguvu na kulala fofofo akiwa na viatu na nguo zake zote. Kwa mbali kabisa, moyo wake ulilia na kuomboleza.
“Uko wapi mpenzi wangu, kwa nini umeniacha peke yangu leo? Ina maana hukunipenda hata kidogo kiasi cha kuamua kunifanyia hivi?
“Najua sitampata msichana mwingine mzuri kama wewe...Ooh Carolina! Nini nimefanya hadi kustahili adhabu hii?”
***
Asubuhi iliyofuata, Dedan aliamka kama kawaida yake na kufungua ofisi yake, kibanda kidogo pembezoni mwa nyumba kubwa aliyopanga, akiuza vifaa vya simu, kuchajisha simu, kutengeneza na kuingiza nyimbo kwenye simu kwa kutumia kompyuta.
Kwa maisha ya kujinyima na kutopenda starehe, kazi yake hii ilimnufaisha kiasi cha angalau kujikimu kimaisha na pengine kumfanya hata asiwaze kabisa kufikiria kufanya kazi nyingine yoyote.
Tofauti na siku nyingine, siku hiyo ilianza vizuri sana kwa upande wake, alipata wateja wengi kupita kiasi. Kama mjasiriamali mwingine mzoefu, alifanya kazi zake kwa umakini mkubwa na kuhakikisha wateja wake wanavutiwa na huduma zake kwa kuongeza ukarimu na kuongea lugha yenye bashasha na hata ikamlazimu kuwajua na kuwaita kwa majina wateja wake ambao walijipanga kwa michapo ya hapa na pale huku akiendelea kuwahudumia.
Hakika mtu yeyote alijisikia huru kukaa kwenye benchi dogo lililopo pembeni ya kibanda cha Dedan, akipiga soga na kupoteza muda, akinywa kahawa au pengine akijiunga na kikundi cha vijana wachache kwenye vikao visivyo rasmi wakibadilishana mawazo ya siku.
Ndiyo, kila mtu hulalamikia ugumu wa maisha wa siku hizi, kiasi cha furaha au jambo jema kutokea kwa nadra sana na pengine lisitokee kabisa hata kufikia mtu kukushirikisha walau punje ya neema yake.
Umasikini ulisababisha kila mtu ajifungie peke yake kwa uchoyo akila matunda ya kazi zake. Hivyo, iwe asubuhi, mchana au jioni, wakazi wa Mtaa wa Songasonga hukutana kwa unyonge si kwa jambo lingine, bali kuzungumzia mawazo dhaifu ya siasa za kupindua nchi na mara nyingine wakisimuliana hadithi za nani kafanya nini, lini na wapi!
Kwa kifupi Dedan alikuwa ndiyo kitovu cha mkusanyiko wa watu katika mtaa mzima wa Songasonga. Kwa sababu hiyo na sifa nyingine kedekede, alitokea kupendwa na kila rika kiasi cha kujulikana vizuri na kila mtu mtaani kwake.
Japokuwa alionekana mwenye furaha kubwa machoni mwa watu siku hiyo, ndani ya moyo wake kwa kificho alikuwa amebeba maumivu makali kiasi kwamba kama hali hiyo ingemkuta mtu mwingine kwa hakika asingekuwa hata na nguvu ya kusimama na kuongea kwa furaha mbele za watu.
Siku zote Dedan aliamini katika kuyamaliza matatizo yake yeye mwenyewe bila kuathiri mwenendo wa shughuli zake au wa watu wengine. Akaamua kutowashirikisha kabisa ndugu wala marafiki zake majonzi na matatizo yake. Mara nyingine aliweza hata kulala na njaa bila kusema wala kuomba msaada kwa mtu yeyote.
Huenda misimamo hiyo ndiyo sababu kubwa iliyomfanya ajikaushe muda wote huo, akiigiza kucheka na watu hali moyoni akilia kwa sauti akimuwaza mpenzi wake, hapana, aliyekuwa mpenzi wake, zamani
“...ooh! Carolina, maisha gani nitaishi bila wewe? Naumia…naumia, ee… Mungu naomba nirudishie Caro wangu.”
Tenzi zilipokwamia hapo alitamani kupiga kelele na kulia kwa nguvu. Huenda angepunguza maumivu walau kwa kiasi kidogo, si ndiyo wanavyosema hao wanaojiita wanasaikolojia, eti kulia kunapunguza msongo wa huzuni na kulainisha mrundikano wa dukuduku lililofungamana rohoni. Waongo wakubwa!
Kinyume na wote hao yeye aliamini kulia si punguzo wala suluhisho la matatizo yake, hasahasa tatizo la mapenzi. Alihakikisha kwamba hatoi mwanya wa hata chozi moja kumdondoka wala kumlengalenga kutoka machoni mwake. Mwanaume rijali hamlilii demu bwana!
Itaendelea Kesho Muda Kama Huu..
USISAHAU KULIKE PAGE YETU KUUNGANA NASI
www.facebook.com/bongochoice
Share, Like Na Comment Ilinijue kama Kunawafwatiliaji Nitume Nyingine.. Asantee....

Changia Maoni Yako Hapa

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright Bongo Choice | Modified By Bongo Choices
Back To Top