GO9G3451
Wizara ya Mawasiliano Sayansi na Teknolojia inajiandaa kupeleka bungeni muswada wa sheria ya makosa ya mtandao 2015 ambayo unaweza kuisoma kwa kubofya hapa. Kama zilivyo sheria nyingi kabla ya kupitishwa wabunge hupewa nafasi ya kuijadili na kufanya marekebisho pale penye mapungufu.  Baada ya kuipitia haraka haraka nimegundua baadhi ya vitu ambavyo naamini havijakaa sawa na nimejaribu kuelezea kwa chini yake. Ni matumaini yangu wabunge wetu wataipitia vizuri zaidi na kugundua mengi ambayo sijayaona.
Endelea kusoma:
Kutoa taarifa za uongo. 16. Mtu yeyote anayetoa taarifa, data au maelezo kwa njia ya picha, uongo maandishi, alama au aina nyingine yoyote kwenye mfumo wa kompyuta, endapo taarifa, data, au maelezo hayo ni ya uongo, yanapotosha au yasiyo sahihi, atakuwa ametenda kosa, na akipatikana na hatia atalipa faini isiyopungua shilingi milioni tatu au kutumikia adhabu ya kifungo kisichopungua miezi sita au vyote.
Sheria hii ina mapungufu, kumbuka kazi mojawapo ya mtandao ni kuelimishana na katika kufanya hivyo takwimu nyingine zinazopatikana zinaweza zisiwe kweli lakini kwa kutofahamu mhusika akazitumia. Lazima kiwepo kipengele kinachomlinda mtu wa aina hii.
Unyanyasaji kwa kupitia mtandao 23.-(1) Mtu hataanzisha au kukadimisha mawasiliano yoyote ya kielektroniki kwenda kwa mtu yoyote kwa kutumia mfumo wa kompyuta, kwa lengo la kurubuni, kulazimisha, kutisha au kunyanyasa au kusababisha maudhi ya hisia. (2) Mtu akataye kiuka kifungu kidogo cha (1) atakuwa ametenda kosa na atawajibika, iwapo atatiwa hatiani, kulipa faini isiyopungua shilingi milioni tatu au kutumikia kifungo kwa kipindi cha kisichopungua mwaka mmoja au vyote.
Haiingii akilini mtu ambaye anatenda kosa kama hili kupewa kifungo cha mwaka mmoja tu au faini ya milioni . Kuna watu wanajidhuru miili yao kwa ajili ya manyanyaso ya mitandaoni kutoka kwa watu waliowaamini ambao baadae wanasaliti uaminifu wao. Kuna haja ya kuongeza muda wa kifungo na kiasi cha faini ikibidi iwepo na kipengele cha fidia kwa mhanga wa kosa hili.
Ukiukaji wa haki bunifu 24.-(1) Mtu hatatumia mfumo wa kompyuta kwa lengo la kukiuka haki bunifu zinazolindwa na Sheria nyingine yoyote. (2) Mtu akatayekiuka kifungu kidogo cha (1) atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani, atawajibika iwapo ukiukaji – (a) hauhusiani na masuala ya kibiashara, kulipa faini isiyo pungua shilingi milioni tano au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu au vyote; (b) unagusa masuala ya kibiashara, kulipa faini isiyo pungua shilingi milioni ishirini au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miaka mitano au vyote.
Sielewi COSOTA, BASATA au Bodi ya Filamu wameshirikishwa kiasi gani katika utungaji wa hiki kipengele.  Kumbuka kutumia kazi ya mtu mwingine kujiingizia kipato unamtia hasara, adhabu haijahusisha kufidia hasara iliyosababishwa na ukikukwaji wa sheria hii badala yake imewekwa faini ambayo ni rahisi sana kuilipa hasa kama umejineemesha vya kutosha kupitia kazi yenyewe. Mfano: Wanaotoa nakala feki za bongomuvi wanaingiza mamilioni kila siku kwa kuzisambaza ndani nan je ya nchi na hata kuzikodisha hawawezi kushindwa kulipa faini rahisi hivyo.
Jaribio la kufanya uhalifu 26.-(1) Pale ambapo mtu anayekusudia kutenda kosa anaanza kutekeleza kusudio lake na anadhihirisha kusudio lake kwa kitendo kinachoashiria kosa, isipokuwa hatekelezi kusudio lake kwa kiasi cha kutenda kosa hilo, atachukuliwa kuwa ametenda kosa hilo. (2) Kwa madhumuni ya kifungu hiki- (a) isipokuwa kwa kiasi cha adhabu haitajalisha iwapo- (i) mkosaji anatenda yote ambayo ni muhimu kwa utendaji wa kosa; au (ii) utekelezaji wa kusudio lake kwa ukamilifu unazuiliwa na mazingira ambayo hayaingiliani na kusudio lake; au (iii) anaacha kutekeleza kusudio lake kwa hiari yake mwenyewe; (b) kutokana na sababu za mazingira yasiyojulikana kwa mhalifu haiwezekani kutenda kosa. (3) Mtu yeyote anayejaribu kutenda kosa chini ya sheria hii atakua ametenda kosa na akitiwa hatiani atawajibika kulipa faini isiyopungua shilingi milioni moja au kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi sita au vyote.
Kula njama ya kutenda kosa 27. Mtu anayekula njama na mtu mwingine kutenda kosa chini ya Sheria hii, anatenda kosa na iwapo atatiwa hatiani, atawajibika kulipa faini isiyopungua shilingi milioni moja au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja au vyote.
Haieleweki itajulikana vipi mtu ALIKUSUDIA kula hivyo kutoa mwanya kwa watu kubambikiwa kesi pale wanapoenda kinyume na matakwa ya watu fulani. Hii inatokea mara nyingi sana na tumeshuhudia ikithibitishwa watu wameuziwa kesi huku wale wasio na wanasheria wazuri wa kuwatetea wakiishia kuingizwa hatiani.
Ulinzi wa miundo mbinu muhimu ya TEHAMA 28.-(1) Waziri anaweza, kwa amri itakayochapishwa kwenye Gazeti la Serikali kuainisha mifumo ya kompyuta kama miundombinu muhimu
(2) Amri iliyorejewa chini ya kifungu kidogo cha (1) inaweza kuainisha vigezo, miongozo na taratibu kuhusiana na- (a) usajili, ulinzi au utunzaji; (b) usimamizi wa jumla; (c) kuingia, kuhamisha na kudhibiti data; (d) kuhakikisha uwepo wa audilifu au uhalali wa data au taarifa; (e) njia zitakazotumika kuhifadhi au kutunza data; (f) mipango ya kudhibiti majanga iwapo kutatokea uharibifu; (g) namna na utaratibu wa kuendesha ukaguzi; (h) jambo jingine lolote ambalo ni muhimu kwa ulinzi, usimamizi na udhibiti wa data na rasimali nyingine. (3) Kwa madhumuni ya kifungu
 –  Waziri amepewa madaraka makubwa sana katika hili ikimpa nafasi ya kuingia katika mifumo ya kompyuta na kufanya yaliyotajwa hapo juu. Katika wakati tulionao kisiasa ambapo kuna wimbi kubwa la wafanyabiashara katika siasa sitoshangaa mmoja ya mawaziri ambaye ana maslahi kibiashara katika mawasiliano au biashara nyingine inayohusiana na tasnia hii kutumia madaraka haya kujinufaisha au kuwanufaisha washirika wake kupitia sheria hii. Ninadhani madaraka haya angepewa mkuu wa kitengo cha Cyber Crime na sio MWANASIASA.
Kufifilisha kosa 50.-(1) Bila kuathiri sheria nyingine inayotumika Tanzania Bara, Mkurugenzi wa Mashtaka, muda wowote kabla ya mwenendo wa mahakama kuanza na kwa kuzingatia tamko la kukiri kosa kwa hiari la mshitakiwa anaweza kufifilisha kosa na kuamuru mtu huyo alipe kiasi cha pesa atakachokitaja ambacho hakitazidi kiasi cha faini kwa kosa hilo.
(2) Amri ya kufifilisha kosa chini ya kifungu kidogo cha (1) itakuwa –
(a) ya maandishi, ikiainisha kosa lililotendeka, kiasi cha fedha zitakazolipwa na tarehe ya kufanya malipo ikiambatanisha tamko la kukubali kosa lililorejewa chini ya kifungu kidogo cha (1);
 (b) ni uamuzi wa mwisho na hautakatiwa rufaa; na
(c) na uwezo wa kutekelezwa katika namna sawa na amri ya Mahakama Kuu.
Naamini rufaa ni haki ya kila mtuhumiwa anaeamini hakutendewa haki. Kusema hukumu itokanayo na makosa ni ya mwisho bila haki ya rufaa ni kukiuka haki ya msingi. Kuna haja ya kurekebisha hili.
NYONGEZA
Muswada haujabainisha wafichuaji maovu “whistle blowers” wanalindwa vipi katika sheria hii kutoka vipengele vinavyoonekana kuwalenga watu ambao ni chanzo cha habari kwa kigezo cha “kutishia usalama wa nchi”. Nchi za wenzetu wanaamini demokrasia ni pamoja na uhuru wa kufichua habari ambazo zina manufaa kwa umma na wanatunga sheria za kuwalinda.
Hayo ndio mapungufu niliyoyaona. Kama kuna una kingine ambacho unaamini kinafaa kurekebishwa tafadhali weka katika comment..