Watu 18 wamekufa papo hapo kwa kuteketea
kwa moto na wengine 11 wamejeruhiwa vibaya kutokana na basi walilokuwa
wakisafiria kugongana na lori aina ya Mitsubishi Fuso, katika kijiji cha
Msimba tarafa ya Mikumi, barabara kuu ya Morogoro – Mbeya.
Ajali hiyo imehusisha basi la Kampuni ya
Nganga linalofanya safari zake kutoka Wilaya ya Kilombero kuelekea
mkoani Mbeya na kugongana na lori hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro,
Leonald Paulo alisema ajali hiyo ilitokea jana saa mbili asubuhi katika
eneo hilo huku likihusisha basi aina ya Scania lenye namba za usajili
T373 DAH na Fuso lenye namba za usajili T164 BKG.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva
wa basi la Nganga ambaye alikuwa katika mwendo kasi na kulipita gari
lililokuwa mbele yake bila ya tahadhari na kukutana na lori hilo na
kisha kugongana nalo katika eneo hilo.
Alisema baada ya magari hayo kugongana,
ndani ya buti ya basi kulikuwa kumepakiwa pikipiki ambayo ilikuwa na
mafuta na baada ya kutokea ajali hiyo kulitokea mlipuko wa moto na
kusababisha basi hilo pamoja na lori kuwaka moto.
Kamanda huyo alisema kuwa kutokana na
moto huo, baadhi ya abiria waliokuwepo katika basi hilo walishindwa
kujiokoa na hivyo miili yao kuteketea kabisa na moto huo, wakiwemo
madereva wote wa magari hayo.
Alisema majeruhi 11 wa ajali hiyo
wamekimbizwa katika Hospitali ya Mtakatifu Kizito iliyopo tarafa ya hiyo
Mikumi kupatiwa matibabu huku hali zao akieleza kuwa baadhi yao ni
mbaya kutokana na kuungua vibaya kwa moto.
Kamanda huyo alisema miili ya marehemu
hao imehifadhiwa katika hospitali hiyo ambapo mpaka sasa haijatambulika
majina yake, licha ya madereva wa magari yote kufa.
Hata hivyo, Kamanda huyo alishindwa
kutaja majina ya majeruhi kutokana na baadhi yao kuendelea kupatiwa
matibabu kwa ajili ya kuokoa maisha yao.
Naye Mganga wa Hospitali ya Mtakatifu
Kizito iliyopo Mikumi, Dk Boniventure Buyagabuyaga, alithibitisha
kupokea jumla ya miili ya marehemu 18 ambao walikuwa wameteketea vibaya
kwa moto kutokana na ajali, ambapo alisema tayari imehifadhiwa katika
chumba cha kuhifadhiwa maiti kwa ajili ya kusubiri utambuzi.
Alisema mpaka sasa majeruhi wanaotibiwa
katika hospitali yake wamebaki saba, lakini hali zao bado ni mbaya
kutokana na kuungua moto katika sehemu mbalimbali za miili yao.
Ajali hiyo imekuwa sawa na mwendelezo wa
ajali za mabasi nchini, kwani Alhamisi iliyopita watu 12 walikufa
katika ajali zilizotokea Tanga na Morogoro, huku wengine wanne waliokuwa
wakisafiri kwa basi la Nyehunge wakiaga dunia usiku wa Jumamosi mkoani
Dodoma.
Katika ajali iliyotokea mkoani Tanga,
katika kijiji cha Mbweni Mkata, majira ya asubuhi, ilihusisha basi la
Kampuni ya Ratco ya Tanga liligongana uso kwa uso na basi la kampuni ya
Ngorika na gari dogo aina ya Toyota Passo na kusababisha vifo vya watu
10 papo hapo, akiwemo mmiliki wa gari dogo, Musa Lupatu aliyekuwa Mbunge
wa zamani wa Korogwe Vijijini.
Katika tukio la Morogoro, watu wawili
walikufa na wengine 48 kujeruhiwa katika ajali iliyosababishwa na basi
la Happy Nation lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Mbeya na kupata
ajali eneo la Mikumi.
Aidha, Machi 12, mwaka huu mkoani
Iringa, basi la Majinja Express lilikuwa likitokea Mbeya kwenda Dar es
Salaam liligongana na lori na kisha likaangukiwa na kontena
lililosababisha vifo vya watu 43.
Post a Comment